Monday, 16 June 2014

RUNGWE NA MAAJABU YAKE

                                                                             Daraja la Mungu

WILAYA ya Rungwe Jijini Mbeya ina mambo mengi ya kustaajabisha na miongoni mwa mambo hayo yapo kwenye Mto Kiwira.

 Mto Kiwira ni mojawapo ya mito minne inayotoka Mlima Rungwe kupeleka maji kwenye Ziwa Nyasa. Mito mingine inayopeleka maji kwenye Ziwa Nyasa ni Lufilyo, Mbaka na Songwe, lakini kila mto una sifa za maajabu yanayotofautiana. 

Mto Kiwira unatofautiana na mito mingine kwa mambo mengi yakiwamo ya kuwa mto wenye urefu wa karibu kilometa 70 kutoka chanzo chake kilichopo Mlima Rungwe hadi Ziwa Nyasa na pia upo chini ya ardhi kwa umbali wa karibu kilometa mbili kutoka usawa wa Mji wa Tukuyu ambao ni makao makuu ya wilaya hiyo. 

 Mto Kiwira umepewa jina hilo kutokana na matawi mengi ya mto huo kupitia karibu na Mji Mdogo wa Kiwira ambao ni maarufu kwa kuuza matunda mbalimbali kwa bei poa wilayani Rungwe. Sehemu kubwa ya maji ya mto huo yanaonekana kuwa meupe kutokana na kuwapo kwa maporomoko madogo madogo mengi yanayopitisha maji kwa kasi inayokadiriwa kuwa kilometa 50 kwa saa. Lakini pia yapo mabwawa ya mto huo yaliyotuama kiasi cha watu wegi kujiuliza kama maji yamesimama ama yanaendelea mbele. Kwa upande mwingine, mto huo pia unafanya kazi moja ya kiserikali ya kugawa mpaka wa vijiji katika Wilaya ya Rungwe, na pia unagawa mpaka wa Wilaya za Rungwe na Ileje , Kyela na Ileje kabla ya kuingia Ziwa Nyasa.

 Umbile la Daraja la Mungu 
 Kama ilivyodokezwa hapo juu, Mto Kiwira upo chini zaidi ya ardhi ya Wilaya ya Rungwe na una maajabu mengi, lakini moja wapo ni la kuwapo kwa daraja linaloaminiwa kuwa la Mungu linaunganisha vijiji vya Lugombo na Mboyo Kata ya Lufingo , wilayani Rungwe. 

Daraja hilo limeundwa kwa mwamba wa mawe ukiwa na urefu wa karibu mita 12 na upana wa wastani wa mita tatu. Ukitaka kwenda darajani hapo, ukitokea jijini Mbeya utapita barabara kuu ya Mbeya kwenda Kyela na utateremkia Kijiji cha Kyimo maarufu kwa jina la ‘KK’ ambapo utapata usafiri wa pikipiki au magari ya kukodi kukupeleka kwenye shimo la Mto Kiwira umbali wa kilometa karibu 10 kutoka barabara kuu.

 Katika safari ya kwenda huko utaiona Sekondari ya Iponjola na baada ya hapo utaingia Kijiji cha Lugombo na kuikuta Sekondari ya mchepuo wa Kiingereza ya God’s Bridge ikiwa na jina hilo ili kuenzi Daraja la Mungu. 

 Safari itaendelea ukijionea pia Shule ya Msingi Kibwe na hatimaye ofisi ya Kijiji cha Lugombo kabla ya kuanza mteremko mkali ambao barabara imewekewa lami ili kupunguza madhara kwa vyombo vya usafiri hadi mtoni 

 Ukianza kuukaribia mto, utaona kwa ng’ambo majengo mengi mazuri yaliyotuama umbali wa kilometa moja chini ya miti pembezoni mwa Mto Kiwira. 

Majengo hayo ni ya Chuo cha Askari Magereza Tanzania .Kwa asilimia kubwa majengo ya chuo hicho yapo pembezoni ya Mto Kiwira , lakini kabla ya kuuvuka mto kupitia daraja lillilojengwa na Serikali utapinda kushoto kuekelea kwenye Daraja la Mungu. Baada ya mita 400 hivi utalikuta daraja lingine ambalo linaelezwa kwamba lilijengwa na Warusi waliopewa kazi ya kujenga mtambo wa kufua umeme kwenye maji yaendayo kasi karibu na Daraja la Mungu.

 Ukiwa kwenye daraja hilo utaliona Daraja la Mungu likiwa kusini mwa mto ambalo limeundwa kwa umaridadi wa aina yake. Daraja hilo kwa chini limejikunja kama upinde, lakini juu kukiwa na nafasi yenye upana unaotofautiana, kwani lipo eneo lenye upana wa mita tano na mita mbili. Kwa kweli ni la ajabu kwani hata maji yanavyokatisha eneo hilo yanatisha. 

 Kutisha kwake kunatokana na maji hayo, badala ya kunyoka kulikatisha daraja, yanaelekea kwanza kwenye mwamba uliopo mashariki na kuzunguka kuelekea kaskazini na hatimaye kuelekea kusini yakiwa na kasi ndogo chini ya daraja hilo kabla ya kupokewa tena na poroko lenye kasi linalotoa mvuke wakati wote. 


 Penye poromoko la maji hayo panaelezwa kwamba Serikali iliwatafuta Warusi ili wasaidie kuweka mitambo ya kufua umeme mwaka 1969 hafi 1978 walipofukuzwa kwa saa 24 bila kufanikisha suala hilo. 

 NIVYEMA TUKALITANGAZA MAANA NI KIVUTIO KIKUBWA CHA UTALII NA KIKAWA CHANZO KIKUBWA CHA MAPATO. CHANZO: MALIASILI ZETU via Tabia nchi Blog

Karibu Tanzania, karibu Mbeya

1 comment:

  1. kwa miaka mingi nilikuwa nikisimuliwa juu ya maajabu yà mahali hapo na nlitamani sana kufika. nashukuru mungu ndoto yangu ikatimia, nlienjoy sana mahali hapo. KARIBU PIA UJIONEE KWA MACHO YAKO.

    ReplyDelete

Welcome

Travel makes one modest, You see what a tiny place you occupy in the world. This page is dedicated to promote tourist attractions of MBEYA Tanzania

Ask a question

Name

Email

Question

Submit

Popular Posts