Sunday 22 June 2014

HISTORIA FUPI YA MKOA WA MBEYA

   
Mkoa wa Mbeya ni moja kati ya mikoa minne (4) iliyopo katika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Mikoa mingine ni Rukwa, Iringa na Ruvuma. Mkoa wa Mbeya ulianzishwa mwaka 1961 na ulikuwa ukijulikana kwa jina la ‘Southern Highland Province’ kwa kujumuisha baadhi ya maeneo ya mikoa ya Iringa na Rukwa. Mkoa una eneo la km. za mraba 63,617 Kati ya hizo km. za mraba
61,783 ni za nchi kavu na km. za mraba 1,834 ni eneo la maji.

Kulingana na Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 1967   mkoa ulikuwa na watu 969,053, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002 Mkoa wa Mbeya ulikuwa na jumla ya watu 2,063,328. Kufikia mwaka 2010 mkoa ulikadiriwa kuwa na watu 2,662,156. 

Mkoa wa Mbeya upo kusini magharibi mwa eneo la Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Mkoa upo katika Latitudi kati ya 7º na 9º 31’ kusini ya Ikweta na Longitudo kati ya 32º na 35º mashariki ya Greenwich. Mkoa unapakana na nchi za Zambia na Malawi upande wa kusini, Mkoa wa Rukwa upande wa magharibi, Mikoa ya Tabora na Singida kwa upande wa kaskazini ambapo kwa upande wa mashariki unapakana na Mkoa wa Iringa. Mji wa Tunduma katika Wilaya ya Mbozi na Kasumulu katika Wilaya ya Kyela, hufanya milango ya kuingilia na kutokea nchi za Zambia na Malawi.

Katika enzi za ukoloni wa Waingereza, Mkoa wa Mbeya ulikuwa ukijulikana kwa jina la ‘Southern Highland Province’. Mkoa ulikuwa ukiunganisha baadhi ya maeneo ya mikoa mitatu ya sasa ambayo ni Iringa na Rukwa. Jina la Mbeya limetokana na neno la kisafwa "Ibheya" ambalo maana yake ni chumvi, kutokana  na  wafanyabiashara  kufika  na  kubadilishana  mazao  yao  kwa chumvi. Mji wa kisasa wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927. Wakati huo dhahabu ilianza kupatikana katika milima iliyopo karibu na Mbeya hadi Chunya hivyo Mbeya ulikuwa ni mji wa mapumziko kwa Wazungu kutokana na hali yake nzuri ya hewa. Mkoa huu ni moja kati ya mikoa mikongwe tisa (9) iliyokuwepo mpaka wakati wa uhuru mwaka 1961.


Katika kipindi hicho, makabila makuu katika Mkoa wa Mbeya yalikuwa ni Wasafwa, Wanyakyusa, Wandali, Wasangu, Wamalila, Wanyiha, wakimbu na Wanyamwanga.


Kijiografia, Mkoa ulianzishwa katika maeneo yanayojulikana hivi sasa kama Uhindini, Uzunguni na Majengo. Mji ulipangwa kufuatana na kawaida ya miji ya kikoloni ya Afrika Mashariki kuwa na sehemu tatu zifuatazo;

(i)       Uzunguni kama sehemu ya nyumba za Wazungu na kando yake ofisi za serikali (Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Polisi na Mahakama)

(ii)      Uhindini   kama   mtaa   wa   biashara   uliokuwa   mikononi   mwa wafanyabiashara wenye asili ya Kihindi na Kiingereza;

(iii)     Majengo kama sehemu kwa ajili ya wafanyakazi Waafrika na familia zao.

Kwa upande wa masuala ya kiimani, Mkoa ulikuwa umegawanywa kama ifuatavyo;

(i)       Kanisa Anglikana lililokuwa dhehebu rasmi la Uingereza ambalo lipo chini ya eneo la Uzunguni karibu na ofisi za kiserikali kama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mahakama.

(ii)      Kanisa  la  Moravian  la  mjini  lilijengwa  eneo  la  Majengo  iliyokuwa sehemu kwa ajili ya makazi ya Waafrika.

(iii)     Kanisa Kuu Katoliki lililokuwa maeneo kati ya Uzunguni na Uhindini karibu na Majengo ambalo lilihudumia Wazungu wachache hasa Waeire na Wahindi kutoka Goa na Waafrika wachache.

Kwa upande wa masuala ya uchumi Mkoa wa Mbeya ulitegemea kilimo cha mazao ya chakula yakiwemo mahindi, viazi vitamu, mtama, mpunga na ndizi. Shughuli nyingine zilikuwa ni biashara na viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza zana za kilimo.


Kielimu, shule zilizokuwepo zililenga hasa kutoa elimu kwa watoto wa machifu, wazungu na wahindi. Shule hizi zilikuwa zinamilikiwa na serikali na mashirika ya dini.  Shule za serikali zilijulikana kama ‘Native Authority’ na za mashirika ya dini ziliitwa shule za wamisionari. Waalimu wazalendo walikuwa wachache, wengi wao walikuwa ni wazungu. Misheni ya Rungwe ndiyo pekee iliyokuwa na Chuo cha Elimu katika Mkoa wa Mbeya baada ya uhuru.


Kuhusu huduma za afya, jamii kwa kiasi kikubwa ilikuwa inatumia tiba za kienyeji. Hospitali zilikuwa chache zikitoa huduma bure isipokuwa hospitali za wamisionari.

Historia hii inapatikana katika taarifa ya mkoa wa mbeya miaka (50) ya uhuru.

karibu sana Tanzania, karibu Mbeya

1 comment:

  1. I Love You home sweet Home Mbeya🙏🙏

    ReplyDelete

Welcome

Travel makes one modest, You see what a tiny place you occupy in the world. This page is dedicated to promote tourist attractions of MBEYA Tanzania

Ask a question

Name

Email

Question

Submit

Popular Posts