Sunday, 31 August 2014

SHEREHE YA MATAMBIKO KABILA LA WASAFWA, MSITU WA IGANJO


Kwa mbali ni Msitu wa Iganjo ambao hutumika kama sehemu ya matambiko iliyoko huko igawilo.

kulia ni Muwakilishi John Chilambo, na katikati ni Chifu Rocket Mwanshinga na wasaidizi wake.

 Mh. Joseph Mbilinyi (mbunge wa Jiji la Mbeya) na Chifu wakipiga picha ya pamoja

Picha ya pamoja ya chifu, wasaidizi wake na wageni waalikwa

 Njuga zinazotumika kuchezea ngoma; huvaliwa miguuni ambazo husaidia sana kuleta radha ya ngoma.


Wakina mama wakicheza ngoma ijulikanayo kwa jina la Mbeta

 Wanaume wakicheza Mbeta,

Ishara ya kidoogo inayotumiwa na hao mapacha, ikimaanisha "kukumbukwa angalau kidogo"  hasa ikiwalenga viongozi

mapacha wakiwa na Mh. Joseph Mbilinyi, na muwakilishi wa mbeya home of tourism modesto
Ngoma ya kisafwa inayo fanyika mwezi wa nane kila baada ya miaka miwili na inahusisha vitu vifuatavyo:-

  • kuwakumbuka ndugu waliokufa
  • matambiko kama kuomba mvua, amani uchaguzi, magojwa biashara na mengine
  • sherehe inayohusisha wasafwa wote na wageni waalikwa kufurahi kwa pamoja.
  • hotuba ya chifu 
Sherehe hio huongozwa na chifu (mwene) wa kisafwa anaetambulika kwa jina la Mwene Rocketi Mwanshinga ambaye ndio chifu mkuu wa wasafwa wote.  chifu huyu alisema tangu apate uchifu huo hajawahi kunyoa nywele

Pia sherehe hiyo hufanyika katika msitu uitwao Iganjo upatikanao maeneo ya Uyole Igawilo. Msitu huo unalindwa kijadi na unamaajabu mengi sana kuna sehemu ambazo huruhusiwi kupiga picha kwa sababu ya taratibu za msitu huo.

Wageni mbalimbali huarikwa katika sherehe hizo bila kujali kabila wala dini.


Karibu Tanzania karibu Mbeya.

MAJI MOTO KILAMBO.

Nlipofika eneo hili nikajaribu kuweka vidole katika maji na nkakuta ni ya moto kiasi kwamba huwezi kuvumilia kuweka vidole ndani ya maji yale kwa muda mrefu.
Haka ni kashimo kadogo lakini ukiangalia maji yake yanatokota kama maji yaliyochemka kwa mda mrefu motoni. 
 Hii ni chem chem inayorusha maji nayo ni ya moto sana.

 Ukiangalia vizuri maji haya kama pana mvuke, ni kutokana na kuwa ya moto hivyo yanatoa mvuke.

Kwa mbali ni muonekano wa eneo la maji moto.

Maji moto haya yanapatikana katika Halmashauri ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe katika eneo maarufu kwa jina la Kilambo lakini ni kijiji cha ikapu ambacho kimepakana na Mbambo. Kilambo ni neno la kinyakyusa lenye maana ya Magadi.

Maji haya ukiyanywa yana radha ya chumvi kitu ambacho kimepelekea sehemu kubwa ya wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani kwenda kunywesha ng'ombe zao maji, Tulikutana na watu kutoka makete, lusungo, lufilyo, mbigili, ikama, mbande, busoka, kasyabone wakiwa na ng'ombe zao. jambo la ajabu ni kwamba mifugo hiyo ikikaribia kufika maeneo hayo hukimbia na huongoza yenyewe kuelekea hapo Muda mwingine wanadai ng'ombe huweza kutoroka zizini ili wakanywe maji yale.

Sehemu hii inavijisehemu vitano, ambapo sehemu za mwanzo maji chumvi yake si kali sana lakini sehemu ya mwisho ni kali sana na ndipo hapo mifugo mingi hupendelea kunywa, Katika chanzo maji ni ya moto yenye uwezo wa kuchemsha yai kwa muda mfupi sana yakishuka kidogo yanakuwa ya vuguvugu na yakiungana na mto uliopita eneo hilo huwa yabaridi kabisa.

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya.
Saturday, 30 August 2014

NAIJUA MBEYA KULIKO WEWE


Mtandao wetu unatambua umuhimu/ mchango wa kila mwananchi katika kukuza utalii wa mkoa wa Mbeya, hivyo umeandaa programu itakayo kwenda kwa jina la NAIJUA MBEYA KULIKO WEWE, Mimi kwanza.

Mtandao huu unatoa nafasi kwa mtu yeyote kutuma picha za kivutio chochote cha kitalii katika mkoa wa mbeya alicho tembelea katika barua pepe mbeyahomeoftourism2@gmail.com au inbox ya facebook page yetu.

Picha zitakazo tumwa ziambatane na taarifa muhimu kama vile wapi mhusika alitembelea na alipenda nini katika maeneo hayo na je nini ushauri wako juu ya sehemu uliyotembelea. kisha mtandao huu utazirusha katika blog yetu na facebook page yetu.

Jivunie Kuwa wa kwanza kuijua mbeya kuliko mwingine yeyote, Sema mimi kwanza.....!!

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya.

SEMINA YA KUJALI MTEJA ILIYOANDALIWA NA MRADI WA SPANEST.

Mratibu wa mradi wa SPANEST Godwell Ole Meing'ataki akimkaribisha mgeni rasmi 

Picha ya pamoja, kulia ni mratibu wa mradi wa SPANEST katikati mgeni rasmi na kushoto Mkufunzi Gosbert Kakiziba

mgeni rasmi akichukua kifungua kinywa 

Mkufunzi Gosbert Kakiziba akiwa anafundisha

 baadhi ya washiriki wakisiliza semina

 mwakilishi wetu Modesto Winfred akiwa katika semina

Jackline na Getrude wakipata maelezo juu ya mbeya home of tourism kutoka kwa modesto mara baada ya chakula.

Semina ya KUJALI MTEJA (Customer care) iliyoandaliwa na mradi wa SPANEST(
Strengthening Protected Areas Network in Southern Tanzania) kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa mbeya iliyofanyika siku mbili tarehe 26 na 27/08/2014 katika ukumbi wa Mtenda Sun Set Hotel iliyopo Soweto Mbeya.

 Katika semina hii tuliweza kujifunza mambo mengi katika maada nne (4) ambazo ni :-
  1. Huduma kwa njia ya mawasiliano
  2.  Kujali Saikolojia ya mteja
  3. Kujenga Uhusiano na 
  4. Wateja na Kujali wateja na kutawala Hisia zao. 
Maada hizi zilifundishwa na Mkufunzi Gosbert Kakiziba kutoka ISHIMA Co operation, tulipozungumza na waliohudhuria karibia asilimia kubwa walisema walinufaika sana na mafunzo hayo hivyo kuomba yaweze kuwa endelevu hata katika halmashauri zingine za jiji la Mbeya. 

Mafunzo haya yalihudhuriwa na taasisi za kiserikali na zile za binafsi lengo kuu ikiwa ni kuwezesha washiriki kukuza uwezo wa kutoa huduma zitakazo wezesha mkoa wa Mbeya kukua kiuchumi, pia kuufanya mkoa wa Mbeya kuwa kitovu cha uchumi, kukua katika sekta ya utalii, chaguo la kwanza kwa uwekezaji, chanzo cha ajira, na kitovu cha weredi na ukarimu katika kutoa huduma.

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya.

Monday, 25 August 2014

MTI MKUBWA WA MASOKO NA MAAJABU YAKE.

Baraka akiwa anapima mti huu na hapa ndipo tulipoanzia kupima.

kufika hapa kipimio chetu kikawa kimeisha ambapo kina futi 16, kisha kupima tena kwa kuanzia hapo.

Tukaanza tena mzunguko mwingine ambao nao uliisha.

Sehemu ya chini ya mti ambayo ukigonga imekuwa ngumi mithiri ya jiwe.

Muonekano wa mti kwa mbali.

Mti huu ni aina ya Mvule na unapatikana masoko katika wilaya ya rungwe, mti huu ni mkubwa kiasi kwamba ili kuweza kuuzunguka wote unahitaji watu kuanzia nane waliounganisha mikono. ukiupima una futi 39 katika kimo cha juu kidogo lakini una futi 43 chini kabisa. Mwenyeji wetu bwana Mwambuga anasema mti huu ni wa kale sana kiasi kwamba hawakumbuki hasa ni wa miaka gani lakini walioweza kutunza angalau historia ni kuanzia karne ya 13 lakini nao waliukuta ukiwa mkubwa sana

Mnamo mwaka 1975 mti huu kwa mara ya kwanza ulidondosha tawi lake moja ambalo hata ukifika inaonyesha maana pana onekana ni wapi hasa lilikuwepo na inasemekana lilipoanguka ilikuwa kama tetemeko la ardhi kutokana na kishindo kilichotetemesha kijiji kile na vijiji jirani.

Katika tawi la kwanza kuna sehemu ya mti huu kutokana na kuwa njia ya kutolea maji ule utomvu wake wa muda mrefu umejikusanya na umefanya umbo lenye muonekano wa pembe hivyo wenyeji huita eneo lile LUPEMBE, sehemu hiyo yanadondoka maji tone moja moja kama yadondokavyo katika dripu na rangi ya maji hayo ni mekundu kiasi kwamba baadhi ya watu huamini kuwa ni damu iliyotumika kama mazindiko hapo zamani. lakini mwenyeji anasema kuanzia karne hiyo ya 13 wanavyoelezwa hakukuwa na matambiko yoyote labda kabla ya karne hiyo, na asilimia kubwa ya matawi ya mti huu yana nyuki,karibu utembelee maeneo haya uweze kujifunza mengi

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya.
Saturday, 23 August 2014

KIKAO CHA ZIARA YA KUPANDA MLIMA LOLEZA KATIKA JIJI LA MBEYA

Volustin mdee kutoka mbeya living lab.


Elly bonke akitoa muongozo wa kikao.
 Picha ya pamoja kwa taasisi zilizoshiriki.

Kikao kilichofanyika mabatini katika ofisi za YWCA kiliudhuriwa na taasisi kadhaa na yafuatayo ndio yalikuwa maafikiano yao ili kufanikisha tukio zima.

KAULI MBIU YETU:”NITASIMAMA, NITATETEA, KIZAZI KIPYA CHA VIJANA, UTHUBUTU UNAANZIA NYUMBANI”

Vijana wa kikundi cha MLIMANI YOUTH GROUP kwa kushirilikiana na taasisi mbalimbali za hapa jiji Mbeya, YWCA MBEYA, EGY BUSINESS SOLUTION, T-MOTIONS,YMCA MBEYA, MBEYA HOME OF TOURISM, MBEYA LIVING LAB, FRESOWE, HALMASHAURI YA JIJI,RESTLESS,VIJANA MBEYA,ORANGE FILMS, SKAUTI MKOA MBEYA,WISE AND MERCY, kwa pamoja kama vikundi vya vijana tukiwa tunajishughulisha na masuala ya kijamii, tumeiandaa kampeni kuu ya vijana Mbeya kwa mwaka 2014 kwa lengo la kuhamasisha jamii katika mambo makuu manne

1. UTHUBUTU WA VIJANA KATIKA CHANGAMOTO ZA MAISHA
Ziara yetu katika kupanda mlima LOLEZA siku ya tarehe 6/9/2014 tumelenga jambo kubwa ni kuhamasisha vijana katika kujifunza na kujiwekea uthubutu katika kuanzisha mambo yenye tija katika jamii hususani kwa vijana kutumia fursa zinazotuzunguka na namna tunavyoweza kujiajiri na kuvumbua vipaji vingi vilivyomo ndani yetu kama vijana.

Tutakuwa na mafunzo na mijadara ambayo tutakuwa tukijadiri katika mlima huo na baada ya kutoka juu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na semina zetu kama vijana, na kupitia njia za mitandao ya kijamii kwa kueneza ujumbe kwa vijana wengi walioko duniani wapate kujifunza tuliyoyaanzisha vijana

2. UTUNZAJI WA MAZINGIRA NA UJENZI WA VIVUTIO VYA UTALII
Tumedhamilia kama vijana kuweka mazingira yetu vyema kwani ndiyo pekee yanayoweza kuwa ajira kwetu na manufaa kwa kizazi hiki na kijacho nyuma yetu hivyo tutakuwa na zoezi la kuokota maganda ya pipi,kopo za plastic, wakati tukielekea juu ya kilele cha mlima loleza tukiwa na dhumuni kubwa la kuokoa mazingira yetu na kuhamasisha jamii kujali mazingira yetu kwani ndiyo chanzo cha utalii wa Taifa letu

3. kujenga umoja wa vijana jiji Mbeya na dunia kwa ujumla
Katika kufanyika kwa tukio hili la vijana wa jiji la Mbeya kwa pamoja ndiyo utakuwa mwanzo mkubwa wa sisi kama taasisi mbalimbali kuunganisha nguvu ya pamoja katika kutatua shughuli mbalimbali za vijana katika jiji na taifa kwa ujumla


4. KUTAKUWA NA UANDAAJI WA DOCUMENTARY YA KUHAMASISHA VIJANA
Kwa ushirikiano wa taasisi za vijana wa jiji Mbeya tutakuwa na utengenezaji wa documentary, vipeperushi, ambavyo vitaeleza ujumbe ambao kwa mwaka huu vijana tutakuwa tukiujadiri, na hatimaye kuusambaza kwa dunia nzima kwanjia za magazeti,radio, tv, blogs, facebook, na mitandao, ambayo tunaamini inaweza kuifikia jamii kwa ujumla

Wednesday, 20 August 2014

UFAHAMU MMEA UJULIKANAO KAMA UPUPU





Ni moja kati ya mimea ipatikanayo katika maeneo mbali mbali hususani katika mapori, mmea huu hutambaa kama mboga za maboga na tunda lake kimuonekano liko kama maharagwe. mmea huu ukikauka na kwa bahati mbaya unga wake ukagusana na mwili wa binadam ni hatari sana kwani kuwasha kwake kiukweli hakuelezeki.

Upupu unaweza kumdharirisha mtu, unaweza kujikita unatoa nguo zote pasipo kuangalia mazingira, si ajabu kumkuta mtu aliepigwa na upupu kapakaa vumbi walau kupunguza makali yake na ajabu yake ni kwamba ukinawa kwa maji una kawaida ya kuongeza kuwasha.

Kwa wale waliowahi/ wanaoishi kijijini, ama wale waliowahi kupatwa na janga hili la upupu nadhani watakuwa mashuhuda wakubwa juu ya ubaya wa hii kitu, nlipokuwa katika safari zangu nokielekea katika moja ya chanzo cha mto sikuuona upupu ulikuwe mbele yangu, kwa bahati nzuri mwenyeji wangu aliuona kisha akapiga yowe ya kunitaka nisimame maana ndipo nlipokuwa naelekea, ko ningepita nadhani yangekuwa mengine.

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya

NGOMA YA KINYAKYUSA (ING'OMA)

Watu wa ndembo.

moja kati ya wachezajia wa Ndembo akionesha umahiri wake wa kucheza kwa mashabiki wake.


wapiga ngoma wa ndembo taratibu wakiingia uwanjani.
wachezaji kutoka maeneo ya lufilyo.
hapo fimbo zilikuwa zikizungushwa kwa umaridadi mkubwa sana.

moja kati ya watu walioufurahisha umati mkubwa wa watu kwa kucheza huku wakiuzunguka uwanja.
Ngoma hii ya kitamaduni aina ya LING'OMA imechezwa katika boma la ilopo katika halmashauri ya Busokelo, wilaya ya Rungwe. imehusisha washiriki wawili ambao ni Ndembo na Lufilyo. ni moja kati ya ngoma zilizofana sana hasa kwa umaridadi wa kila kikundi kutaka kuwafurahisha watazamaji.

Aina mbali mbali za ngoma zipatikanazo katika jamii ya kinyakyusa ni pamoja na IPENENGA, AMAGHOSI, ISAMBA na INGOMA, Ngoma hii huchezwa kwa ustadi wa hali ya juu sana na wenye kuvutia mno. Utawakuta wachezaji wamevaa nguo nyeupe pee, zilizotiwa nakshi na wekundu kwa mbali

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya.
Tuesday, 19 August 2014

TANGAZO LA KUPANDA MLIMA LOLEZA.


Safari ya kupanda MLIMA LOLEZA itakayo fanyika Tarehe 06/09/2014 yenye kauli mbiu "NITASIMAMA. NITATETEA, KIZAZI KIPYA CHA VIJANA UTHUBUTU UNAANZIA NYUMBANI' imeandaliwa na MLIMANI YOUTH GROUP, ambao wameshirikiana na taasisi/ asasi mbalimbali za vijana wakilenga mambo makuu matatu

1. UTUNZAJI WA MAZINGIRA NA UJENZI WA UTALII KATIKA MKOA WETU.
2.KUHAMASISHA VIJANA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO ZA KIMAISHA HUSUSANI KUWA NA UBUNIFU
3.KUJENGA UMOJA BAINA YA TAASISI NA VIJANA JIJINI MBEYA, 


Ahsante kwa mulionesha nia ya kushiriki, mwanzo tuliweka idadi ya watu 40, sasa imefikia 50 na ndiyo mwisho, ili kuthibitisha jina lako ama kwa anetaka kudhamini wasiliana na event coordinator 0764 761 900 ELLY BONKE


Asasi zitakazo shiriki ni pamoja na MBEYA YOUTH DEVELOPMENT NETWORK (VIJANA MBEYA), CHAMA CHA SKAUTI MKOA WA MBEYA, RESTLESS, WISE & MERCY COMPANY, TMOTION, MBEYA LIVING LAB, HALMASHAURI YA JIJI, MBEYA HOME OF TOURISM, YWCA, FRESOWE na EGY BUSINESS SOLUTION.

KARIBU TUSHIRIKI PAMOJA.
Saturday, 16 August 2014

JIWE LA AJABU LENYE CHUMA JUU YAKE.









Jiwe hili lipo katika kata ya ilima, nje kidogo ya mji wa Tukuyu katika barabara ielekeayo Kyela, ni jiwe ambalo juu yake kuna chuma ambacho hakijafungwa kwa nati wala kitu chochote lakini hakitikisiki wala hakitoki, inasemekana jiwe hili liliwekwa enzi za ukoloni na koloni la mwingereza. Miaka kadhaa iliyopita wananchi wa eneo hili walitaka kujua chini ya jiwe kuna nini? ndipo walipoamua kuchimba ili kujua kuna nini lakini hawakukuta kitu chochote.

Baada ya kukuta hakuna kitu chochote ndipo walipotaka kuliangusha ili lisiwepo kabisa walijaribu kutaka kuliangusha pasipo mafanikio kwa sababu halikuonesha mwisho wake ni wape kwa kwenda chini.

Karibu Tanzania, Karibu Mbeya.

Welcome

Travel makes one modest, You see what a tiny place you occupy in the world. This page is dedicated to promote tourist attractions of MBEYA Tanzania

Ask a question

Name

Email

Question

Submit

Popular Posts